SHAMBA LA BIBI

SHAMBA LA BIBI

Thursday, 29 October 2015

MAGUFULI ATANGAZWA MSHINDI UCHAGUZI WA URAIS TANZANIA

Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete anayeondoka mamlakani

Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CCM John Pombe Magufuli ndiye rais mteule wa taifa la Tanzania baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.

 

Akitoa matokeo hayo mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Magufuli, ambaye alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa leo, alijipatia kura 8,882,935 ikiwa ni aslimia 58.46 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa wa chama cha Chadema akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote. 

 

Dkt Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959.



Wafuasi wa chama cha CCM wameanza kusherehekea ushindi wa Bw Magufuli

Awali kabla ya kutolewa kwa matokeo hayo vyama vya siasa vilivyokubaliana na matokeo vilitia sahihi matokeo hayo. 

 

Lakini chama cha Chadema, chake Bw Lowassa hakikuwakilishwa, chama hicho kimepinga matokeo hayo.

 

Akivihutubia vyombo vya habari mgombea wa urais kupitia chama hicho Edward Lowassa amepinga matokeo yoyote ya uchaguzi huo na kujitangaza mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 62 ya kura zilizopigwa.

 

Lowassa amedai kwamba tume ya uchaguzi nchini humo imeshirikiana na chama tawala CCM kufanya udanganyifu katika shughuli hiyo, madai ambayo tume hiyo imekanusha.

 

"Hatuna hata chembe ya wasiwasi kwamba mchakato huu ulifuata sheria na ni halali," alisema Jaji Lubuva muda mfupi kabla ya kutangaza matokeo.

 

Aidha, amesema tume iliendesha mchakato wote "bila shinikizo".




Source: BBC swahili.

No comments:

Post a Comment