SHAMBA LA BIBI

SHAMBA LA BIBI

Thursday, 29 October 2015

HISTORIA YA SAMIA SULUHU HASSAN

Historia ya Samia Suluhu Hassan wa CCM

Ushindi wa John Pombe Magufuli wa CCM umetoa fursa kwa Bi Samia Suluhu Hassani kuhudumia taifa hilo la Afrika Mashariki kama mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa rais wa Tanzania.

Lakini Bi Samia ni nani?

 

Tangu kongamano la Chama tawala nchini Tanzania CCM kumteua Daktari John Pombe Magufuli Joseph kuwa mshika bendera wa CCM, Chama hicho kiliweka historia kwa kumteua Bi Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza.

 

Tangu Dodoma, Bi Samia aliwekwa kwenye ramani ya wanasiasa wanawake waliobobea barani Afrika.

 

 

Lakini Bi Samia Suluhu Hassanni Nani ?

 

Bi Samia Suluhu ana umri wa miaka 54.

 

Kwa wale wanaomjua Bi Samia wanasema kuwa ni mchache wa maneno.

Asili yake ni Kisiwani Zanzibar.

 

Bi Samia Suluhu Hassan amewahi kushikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali ya Muungano wa Tanzania na kadhalika amewahi kutumikia serikali ya visiwani Zanzibar kama waziri katika afisi ya makamu wa rais.

 

 

Ni mwanamke wa Kwanza kuwa Mgombea Mwenza

 

Tangazo la kumtaja kama mgombea mwenza wa rais mteule wa tano wa jamhuri ya Muungano ya Tanzania sasa limezaa matunda na kumuweka Bi Samia katika mstari wa mbele barani Afrika kama naibu rais wa Jamhuri ya Tanzania.

 

Chama CCM pia kimeingia katika daftari la vyama vilivyowapa wanawake sauti katika serikali yake katika karne hii ya 21.

 

Bi Samia alikamilisha masomo ya shule ya upili mwaka wa 1976 .

 

 

Masomo

 

Aliajiriwa kama mchapishaji katika wizara ya mipango na maendeleo ya nchi, kazi ambayo aliifanya huku akiendelea na masomo yake hadi alipohitimu katika chuo kikuu cha Manchester, Uingereza.

 

Bi Samia anasema kuwa njia yake ya ufanisi haijakuwa rahisi kama inavyodhaniwa.

 

''Safari yangu katika siasa imekuwa njia ndefu na yenye tija.''

 

Kimsingi ufanisi wangu katika siasa za Tanzania umetokana na uweledi na umakini katika kila jambo ninalolifanya.''

 

''Sio rahisi kuwajibikia familia yako wakati huohuo ukiendelea na maisha ya siasa elimu na majukumu mengine ya kikazi," anasema Bi Samia.

 

Familia

Aliolewa mwaka wa 1978, kwa Bw Hafidh Ameir, ambaye wakati huo alikuwa afisa wa Kilimo .

Walijaliwa watoto wanne.

 

Mmoja kati ya wanawe Wanu Hafidh Ameir (1982), ni mwakilishi maalum katika bunge la Zanzibar

 

Bi Samia Suluhu Hassan na rais Mteule John Magufuli

Siasa

 

Alijiunga na siasa mwaka wa 2000.

 

Wakati huo alijiunga na bunge la wawakilishi la Zanzibar kama mjumbe maalum.

 

Haikuchukua muda nyota yake ikaanza kung'aa na akateuliwa kuwa waziri na rais Amani Karume.

 

Alitumikia taifa hadi mwaka wa 2005 alipochaguliwa tena na kuteuliwa upya kama waziri.

 

Mwaka wa 2010 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi.

 

Punde tu akateuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa maswala ya muungano.

 

MAGUFULI ATANGAZWA MSHINDI UCHAGUZI WA URAIS TANZANIA

Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete anayeondoka mamlakani

Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CCM John Pombe Magufuli ndiye rais mteule wa taifa la Tanzania baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.

 

Akitoa matokeo hayo mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Magufuli, ambaye alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa leo, alijipatia kura 8,882,935 ikiwa ni aslimia 58.46 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa wa chama cha Chadema akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote. 

 

Dkt Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959.



Wafuasi wa chama cha CCM wameanza kusherehekea ushindi wa Bw Magufuli

Awali kabla ya kutolewa kwa matokeo hayo vyama vya siasa vilivyokubaliana na matokeo vilitia sahihi matokeo hayo. 

 

Lakini chama cha Chadema, chake Bw Lowassa hakikuwakilishwa, chama hicho kimepinga matokeo hayo.

 

Akivihutubia vyombo vya habari mgombea wa urais kupitia chama hicho Edward Lowassa amepinga matokeo yoyote ya uchaguzi huo na kujitangaza mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 62 ya kura zilizopigwa.

 

Lowassa amedai kwamba tume ya uchaguzi nchini humo imeshirikiana na chama tawala CCM kufanya udanganyifu katika shughuli hiyo, madai ambayo tume hiyo imekanusha.

 

"Hatuna hata chembe ya wasiwasi kwamba mchakato huu ulifuata sheria na ni halali," alisema Jaji Lubuva muda mfupi kabla ya kutangaza matokeo.

 

Aidha, amesema tume iliendesha mchakato wote "bila shinikizo".




Source: BBC swahili.

Thursday, 22 October 2015

BASATA, WADAU WAWEKA MIKAKATI KUUPA HADHI MUZIKI WA REGGAE

 

Wadau wa muziki wa reggae nchini kwa kujengewa mazingira na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wameweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha wanaurudisha jukwaani muziki huo na kuainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili.

 

Akizungumza mapema wiki hii kwenye programu maalum iliyolenga kuujadili muziki wa reggae na kuja na mikakati ya kuurudishia hadhi iliyoandaliwa na BASATA, Msanii mkongwe wa muziki huo Innocent Nganyagwa alisema kwamba wasanii wa muziki huo kwa sasa wamejipanga kuurudisha jukwaani muziki huo kupitia kufanya maonesho maeneo mbalimbali nchini. 

 

“Tumejipanga kufanya maonesho ya muziki wa reggae katika mikoa mbalimbali nchini, tutakuwa na kundi la wasanii ambao kazi yao itakuwa kufanya maonesho ya hisani na kuurudisha jukwaani muziki huu ambao kihistoria ni muziki mama” alisema Innocent Nganyagwa.

 

Aliitaja mikoa ambayo maonesho hayo ya reggae yatafanyika kuwa ni pamoja na Mbeya, Ruvuma, Iringa, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na mingine ambayo maandalizi bado yanaendelea ili kuhakikisha wanawafikia wapenzi wengi zaidi wa muziki huu ambao huko nyuma ulipata kuwa na mvuto mkubwa.

 

Mikakati mingine iliyowekwa ukiacha kufanya maonesho mbalimbali nchini ni pamoja na wasanii wa reggae kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika kujitangaza, kuanza kuuza kazi zao kupitia mitandaoni, kubuni kazi zenye ujumbe unaoendana na soko na kuacha kuganda na falsafa ya reggae ni muziki wa ukombozi. 

 

Awali wakibainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili muziki huo, wadau wengi walisema kwamba muziki huu unasuasua kutokana na vituo vingi vya radio kuupa kisogo, watanzania wengi kuuhusisha na imani za urasta kitu ambacho si sahihi na zaidi wadau muhimu hasa makampuni ya biashara kutoujali katika ufadhili.

 

 “Muziki huu wa reggae si wa marasta pekee, bahati mbaya watu wengi wamekuwa wakiuhusisha na imani za kirasta. Hapana. Muziki huu unafanywa na mtu yeyote na ni muziki kama ilivyo miziki mingine” alisema Ras Bumijah Zinyongwa ambaye pia ni kiongozi wa taasisi ya Tanzania Rastafarai Movement (TARAMO)